Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Usafiri
wa Baharini Zanzibar Abdullah Husein Kombo
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar imezifutia rasmi
hati ya kufanya kazi Meli ya Mv.Kalama, Mv.Seagul na Mv.Sepideh kutokana na meli
hizo kutokukidhi hali ya usalama wa abiria katika meli hizo.
Aidha meli hizo zimepewa muda wa mwezi mmoja kuanzia leo
kuhakikisha zimeondoka katika maeneo ya Zanzibar
kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa dhidi ya wamiliki wa Meli hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Usafiri
wa Baharini Zanzibar Abdullah Husein Kombo wakati alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari Afisini kwake kuhusu hali ya usafiri wa baharini na usalama
Zanzibar.
Amesema Mamlaka hiyo imefanya tathmini na uhakiki wa kutosha
na kujiridhisha kuwa Meli hizo hazifai kufanya kazi katika maeneo ya Zanzibar jambo ambalo
limepelekea kuchukua hatua za kufuta hati za kufanyia kazi meli hizo.
Amefahamisha kuwa sababu kuu zilizopelekea Mamlaka kufanya
maamuzi hayo ni pamoja na uchakavu,umri wa meli hizo kuwa mrefu na kupata
matatizo mara kwa mara katika safari zao.
Kombo amefahamisha kuwa Sheria ya Mamlaka ya Usafiri na
Bandari Zanzibar
ya mwaka 2006 kifungu cha 17.1 inampa mamlaka Msajili wa Meli kuifuta meli
yoyote ambayo itakuwa haikidhi usalama wa abiria.
Kufuatia sheria hiyo Kombo amesema watawataka wamiliki wa
Meli hizo kuzirudisha hati za kufanyia kazi meli hizo ili waende kutafuta
sehemu nyengine za usajili kinyume na maeneo ya Zanzibar.
Akizungumzia Meli ya Mv.Serengeti Kombo amesema wamelazimika
kuiagiza meli hiyo kupunguza idadi ya abiria kutoka watu 800 hadi 350 na tani
za mizigo kutoka 100 hadi 50 hadi pale
ambapo watajiridhisha kutokana na hali ya meli hiyo ilivyo.
Na Faki Mjaka-Maelezo
Zanzibar
26/07/2012
No comments:
Post a Comment